28 Februari 2026 - 09:00
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje kuhusu kuongezeka kwa mvutano kati ya Pakistan na Afghanistan

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa ikieleza wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Pakistan na Afghanistan. Iran imezitaka pande zote mbili kuanza mazungumzo ya haraka ili kusitisha mapigano, kuheshimu mamlaka na mipaka ya kila nchi, na kuepuka hatua zinazoweza kuongeza hali ya taharuki. Pia imetangaza utayari wake kusaidia juhudi za kupunguza mvutano na kufanikisha maelewano ya amani.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa kufuatia kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi jirani za Pakistan na Afghanistan.

Ifuatayo ni Andiko Kamili kuhusu Taarifa Hiyo:


Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeeleza wasiwasi na masikitiko yake makubwa kutokana na kuongezeka kwa mapigano kati ya nchi mbili jirani na za Kiislamu, Pakistan na Afghanistan, pamoja na athari zake za kiusalama na kibinadamu. Imetaka kuanza mara moja kwa mazungumzo na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ili kusitisha mapigano na kupunguza mvutano.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mapigano kati ya Pakistan na Afghanistan si tu yamesababisha vifo na hasara za mali kwa nchi hizo mbili jirani, bali pia yanaweza kuongeza ukosefu wa usalama katika eneo zima na kuleta madhara ya kibinadamu na kiusalama kwa kanda nzima.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza upya wito wake kwa pande zote mbili kuheshimu mamlaka ya kitaifa na mipaka ya kila mmoja, na kuepuka hatua yoyote inayoweza kuongeza mvutano na mapigano. Aidha, imetangaza utayari wake wa kusaidia katika kupunguza mvutano na kuwezesha mazungumzo kati ya nchi hizo mbili ili kusitisha kikamilifu mapigano ya kijeshi na kufikia maelewano.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha